Waziri Mkuu Awataka Viongozi Wa Dini Kushirikiana Na Serikali Kupambana Na Rushwa, Ufisadi
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kushirikiana na
Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili
zikiwemo za rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Amesema
siku zote kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Asasi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na madhehebu ya Dini katika kuwapatia huduma
za kijamii kama vile, afya, elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyingi
nyingine.
Waziri
Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana mchana (Jumapili, Juni 12, 2016)
wakati alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli katika Ibada
ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Mhashamu Askofu Flavian Kassala
kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.
“Serikali
inatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Kanisa Katoliki katika Jimbo
hili la Geita na Tanzania kwa ujumla hivyo wito wangu kwa Baba Askofu na
Waumini wa Kanisa kwa ujumla wenu ni kuwaomba muendelee na kazi hii
nzuri ya kutoa huduma muhimu kwa jamii,” alisema.
Alisema
maendeleo ya nchi yanawategemea wote hivyo ushirikiano kati ya Kanisa
na Serikali utawezesha maendeleo ya Taifa kupatikana kwa kasi zaidi na
kunufaisha wananchi wote.
Waziri
Mkuu alisema jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ambayo
yatasaidia Mtanzania kujikomboa na umaskini na kwamba kazi kubwa ya
viongozi wa dini kuunganisha jamii na wala siyo kuwatenganisha.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alisema kinachotakiwa kufanywa na wote ni kumwuomba
Mwenyezi Mungu awawezesha kuwaelewa viongozi walioko madarakani na kutii
maelekezo yanayotolewa kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kutii
mamlaka.
Alisema
iwapo waumini watatii na kuzingatia mafundisho ya kiroho yanayotolewa
na viongozi wao wa dini ni dhahiri kwamba yatajenga imani miongoni mwao
na upendo utatawala katika jamii nzima.
Waziri
Mkuu alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Madhehebu yote katika
kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, hivyo aliwasihi waendelee
kuwekeza katika huduma za jamii ikiwemo Shule, Vyuo, Zahanati kwa kuwa
wana jukumu la kushirikiana kwa pamoja kujenga taifa.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu aliwaomba wote kwa pamoja waunge mkono juhudi za
Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli katika kupambana na uzembe, ubadhirifu na
wote wanao kiuka maadili ya utendaji wa kazi.
Kwa
upande wake Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo la Bunda ambaye alikuwa
msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Geita amewaomba waumini kumpa
ushirikiano Askofu mpya wa jimbo hilo.
IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JUNI 12, 2016.
JUMAPILI, JUNI 12, 2016.
No comments