Rais Magufuli Ahudhuria Ibada Katika Kanisa La Maombezi La Mchungaji Antony Lusekelo ‘Mzee Wa Upako’ Ubungo Kibangu
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amelitembelea Kanisa la Maombezi linaloongozwa na Mchungaji Antony
Lusekelo (Mzee wa Upako) lililopo Ubungo Kibangu Jijini Dar es salaam na
kuwaahidi waumini wa kanisa hilo kuwa Serikali yake itatengeneza
barabara ya kutoka Ubungo Kibangu hadi River Side ambako itaungana na
barabara ya Mandela.
Rais
Magufuli ambaye amezungumza katika ibada ya asubuhi ya Kanisa hilo
iliyofanyika leo tarehe 05 Juni, 2016 amesema amepita katika barabara
hiyo ambayo imekuwa ikitumiwa na waumini wa kanisa hilo na wananchi
wengine wa eneo la Ubungo Kibangu kwa lengo la kujionea hali halisi.
Aidha,
Rais Magufuli amempongeza Kiongozi wa Kanisa hilo Mchungaji Antony
Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako kwa huduma ya maombezi
anayoitoa kwa waumini wake na watazamaji wanaofuatilia vipindi vyake vya
Mahubiri kupitia Luninga.
“Mimi
ni mfuatiliaji mzuri sana wa mahubiri yako, kwa hiyo mahubiri
unapoyatoa yanasambaa, kwa kweli mimi na familia yangu huwa yanatubariki
sana, kwa hiyo nataka kukuthibitishia ninakupenda sana.
“Ndio
maana kuna siku moja, ulizungumza kuhusu shida ya barabara yako ikabidi
nitafute mbinu za namna gani tunaweza kuishughulikia kwa utaratibu ulio
wazi, nikamtuma meneja wa barabara wa Mkoa wa Dar es salaam, akaja,
akaipitia na akafahamu changamoto zilizopo, akafanya upembuzi yakinifu
na usanifu, nataka kukuthibitishia kuwa fedha za kutengenezea barabara
hii zipo” Amesema Dkt. Magufuli huku akishangiliwa na waumini.
Kwa
upande wake Kiongozi wa Kanisa la Maombezi Mchungaji Antony Lusekelo
(Mzee wa Upako) amemshukuru Rais Magufuli kwa kulitembelea kanisa hilo,
na amemuombea heri katika uongozi wake ili aweze kufanikisha azma ya
kuliletea taifa maendeleo ikiwemo mpango wa kuanzisha viwanda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
No comments