Rais Magufuli Mgeni Rasmi siku ya Kimataifa ya Albino
Na: Lilian Lundo- MAELEZO
Mhe.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuongeza uelewa kuhusu ualbino
yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama
cha Watu Wenye Ualbino Nchini (Tanzania Albinism Society) Nemes Temba
ameeleza kuwa kupitia maadhimisho hayo jamii itapata fursa ya kupewa
elimu muhimu kuhusu ualbino ili kuondoka na dhana potofu hususani
ushirikina.
“Maadhimisho
haya ambayo yataanza Juni 11 hadi Juni 13, 2016 yatasindikizwa na mambo
mbalimbali ikiwemo huduma za afya hususani uchunguzi na matibabu ya
saratani ya ngozi pamoja na nasaha za viongozi na mabalozi, utambulisho
wa Miss Albino Tanzania na uzinduzi wa kamusi ya ulemavu,” alisema Temba.
Temba
aliendelea kuainisha kwamba siku hiyo itawapa fursa watoto wenye
ualbino waishio kwenye vituo mbalimbali nchini kutembelea mji wa
Bagamoyo kujionea mambo mbalimbali chini ya ufadhili wa shirika la
UNICEF.
Aidha
Mwenyekiti huyo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kuwapa vipaumbele watu wenye ulemavu akiwemo Dkt. Abdallah Possi ambaye
ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Kazi na Watu
Wenye Ulemavu hii inadhihirisha kuwa ulemavu si hoja bali utendaji kazi
ndio kitu umuhimu.
No comments