TRA Yakusanya Trilioni 1.032 Mwezi wa Tano
Ikiwa imewekewa lengo la kukusanya Sh12.054 kwa kipindi cha Julai 2015
hadi Mei 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kufikia
malengo kwa kukusanya Sh1.032 trilioni kwa kipindi cha mwezi uliopita,
ikiwa ni sawa na asilimia 100.7 ya lengo lililowekwa.
Makusanyo
hayo yanaifanya Serikali ya Awamu ya Tano iliyoingia madarakani Novemba
5, 2015 kukusanya zaidi ya Sh6.567 trilioni katika kipindi cha miezi
mitano. Takwimu zinaonyesha kwamba kuanzia mwezi Desemba, TRA
haijakusanya mapato chini ya Sh1 trilioni.
Akizungumza na
waandishi wa habari mjini Moshi, jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo
Kidata alisema lengo lao kwa mwezi uliopita lilikuwa ni kukusanya
Sh1.025 trilioni na kwamba, kuanzia Julai 2015 hadi Mei 2016 wamekusanya
Sh11.956 trilioni.
“TRA imejiwekea mikakati thabiti ya kuongeza
mapato kwa kipindi cha mwezi mmoja uliobaki ili kuweza kufikia au
kuvuka lengo kwa mwaka huu wa fedha na kwa sehemu kubwa tumeendelea
kupambana na magendo, hususan katika mipaka,” alisema Kidata.
No comments