Bajeti ya Magufuli 2016/17 Hadharani Leo....Macho na Masikio Yote Yaelekezwa Dodoma
TANZANIA kama zilivyo nchi nyingine za Afrika Mashariki, leo inawasilisha bungeni mjini Dodoma Bajeti ya Serikali ili Bunge liijadili na kuipitisha, ianze kutekelezwa katika mwaka mpya wa fedha 2016/17 unaoanza Julai mosi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango anatarajiwa kuiwasilisha bajeti hiyo inayoelezwa kuwa na Sh trilioni saba zaidi ya ile iliyopitishwa na Bunge hilo mwaka jana, ambayo utekelezaji wake unaishia Juni 30, 2016.
Hii
ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John
Magufuli, ambaye ameeleza kuwa anataka kujenga Tanzania ya viwanda,
ambayo nia ni kuifanya iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Tofauti
na bajeti ya mwaka jana ya jumla ya Sh trilioni 22.495 zilizotengwa
kutoka katika vyanzo vya ndani na nje, bajeti nzima ya mwaka huu kwa
mujibu wa mapendekezo ya ukomo wa bajeti hiyo yaliyowasilishwa kwenye
mkutano wa wabunge wote Dar es Salaam, Aprili 6, mwaka huu ni Sh
trilioni 29.539.
Bajeti
hiyo inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania, inatajwa kutokana na vyanzo
mbalimbali vya ndani na nje ambavyo kutokana na mapendekezo hayo ya
awali, serikali imepanga kutumia Sh trilioni 17.719 kwa matumizi ya
kawaida na Sh trilioni 11.82 kwa matumizi ya maendeleo ambayo ni sawa na
asilimia 40 ya mapato ya ndani.
Mapato
ya kodi na yasiyo ya kodi yaliainishwa katika mapendekezo hayo ya
bajeti kuwa ni Sh trilioni 2.693 wakati mapato kutoka Halmashauri yakiwa
ni Sh bilioni 665.4.
Bajeti
hiyo ya mwaka mpya wa fedha inategemewa kujumuisha fungu kutoka kwa
washirika wa maendeleo ambalo ni asilimia 12 tu ya bajeti yote sawa na
Sh trilioni 3.600.
Miongoni
mwa vipaumbele vinavyotajwa kuzingatiwa katika bajeti hiyo ambavyo Dk
Mipango aliwahi kuviainisha ni pamoja na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya
Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka huo mpya wa fedha kwa kipindi cha
miaka mitano.
Vipaumbele
vingine ni viwanda vya kukuza uchumi pamoja na ujenzi wa msingi wa
uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu
na kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara. Lengo la serikali
ni kuhakikisha uchumi unakua kwa asilimia mbili zaidi kufikia asilimia
7.2 badala ya asilimia saba iliyopo.
Inategemewa
pia kuwa mkazo zaidi kwenye bajeti hiyo utawekwa katika kukamilisha
miradi ya maendeleo inayoendelea, miradi mipya, kulipa madeni
yaliyohakikiwa na utekelezaji wa maeneo yote ya vipaumbele
yaliyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka wa fedha unaoisha.
Mchango
wa washirika wa maendeleo katika bajeti hiyo unahusisha misaada na
mikopo, inayojumuisha maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na
kibajeti.
Katika
bajeti inayosomwa leo, serikali imependekeza mikopo ya Sh trilioni
5.374 kutoka katika soko la ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani
zilizoiva pamoja na mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ya
pamoja na kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa.
Aidha,
katika mapendekezo yake ya ukomo wa bajeti hiyo, Dk Mpango alisema
serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 2.11 kutoka kwenye soko la nje
kwa masharti ya kibiashara.
Matarajio
ya ongezeko la makusanyo ya kodi ni kufikia asilimia 12.6 huku
makusanyo ya ndani na Halmashauri yakitegemewa kufikia asilimia 14.8.
Tangu
Aprili 22, mwaka huu, wizara mbalimbali ziliwasilisha makadirio ya
mapato na matumizi yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 zikianzia na Ofisi ya
Waziri Mkuu na kumaliziwa na Wizara ya Fedha na Mipango iliyowasilisha
makadirio yake Juni mosi, mwaka huu.
Kwa
siku sita kuanzia Juni 2, mwaka huu, serikali kwa kushirikiana na
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilikuwa inafanya majumuisho kwa
kuzingatia hoja zenye maslahi kwa Taifa zilizojitokeza wakati wa
kujadili Bajeti za Wizara.
Zipo
changamoto mbalimbali zilizoelezwa na wabunge katika mijadala hiyo ya
Bajeti za Wizara ambazo inatarajiwa kuwa serikali itakuwa imezichukua na
inaweza kuzifanyia marekebisho kupitia Bajeti Kuu leo.
Bajeti
ya leo ambayo itasomwa saa 10 kamili jioni na kuoneshwa moja kwa moja
katika televisheni nchini, itatanguliwa na Taarifa ya Hali ya Uchumi
itakayosomwa na Dk Mpango leo asubuhi.
Kesho
wabunge watapata fursa ya kusoma na kutafakari hotuba hizo mbili kabla
ya Ijumaa kuanza mjadala wake ambao utadumu kwa siku saba hadi Juni 20,
mwaka huu ambayo utahitimishwa kwa uamuzi wa kura.
No comments