CHADEMA Kuishitaki Serikali Kwa Wananchi
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza ziara ya
kuishtaki Serikali kwa wananchi kuhusiana na utumbuaji majipu usiofuata
maadili ya kazi na kutoonyeshwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya
televisheni ya vikao vya Bunge.
Mratibu wa ziara hiyo, Singo
Benson alisema ziara itaanza Juni 7 katika Wilaya ya Kahama mkoani
Shinyanga na kuendelea mikoa mingine, lengo ni kuelimisha wananchi juu
ya ubakwaji wa demokrasia.
“Wananchi wananyimwa haki ya msingi
ya kutoona matangazo ya Bunge moja kwa moja na hakuna sababu ya msingi
iliyotolewa, hivyo lazima tuwaelimishe na tuwatetee wananchi haki zao,”
alisema Benson.
Aliongeza
kuwa katika utumbuaji majipu unaofanyika, umekuwa kwa asilimia kubwa
ukilenga majipu madogo (viongozi wa chini) na kuacha viongozi wakubwa
mafisadi bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Benson
alitoa mfano wa ubakwaji wa demokrasia akisema ni kitendo cha Serikali
kuingilia mihimili mingine, Bunge na Mahakama, ambapo kwa Bunge Serikali
ina daiwa kuingilia uchaguzi wa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali(PAC) ambaye anatakiwa kutoka kambi ya upinzani.
Alisema
ziara hiyo itakayojumuisha Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji itakuwa na awamu nne nchi
nzima huku wabunge wote na wajumbe wakuu wa chama watashiriki, akiwamo
aliyekuwa mgombea urais 2015, Edward Lowassa.
Awamu ya kwanza
itakayochukua siku 14 itaendelea kwa kugawana maeneo na kundi moja la
viongozi wa Chadema litaenda maeneo ya Chato, Katoro, Busanda,
Biharamulo, Muleba, Bukoba Mjini, Karagwe, Ngara na Geita; Kundi la pili
Shinyanga mjini, Meatu, Maswa, Bariadi, Lamadi, Musoma Mjini, Bunda,
Tarime na kuhitimisha Mwanza Mjini.
Benson ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Uratibu na Mafunzo wa Chadema, alieleza kuwa awamu ya pili
itahusisha nyanda za juu kusini na kati, awamu ya tatu itakuwa mikoa ya
kaskazini na kusini na kuhitimisha jijini Dar es Salaam.
“Ziara
hizi zinawakaribishwa wabunge na wanasiasa wa vyama vyote wenye lengo
la kutetea haki za wananchi kwa viongozi waliowachagua,” alieleza
Benson.
No comments