Hotuba ya Zitto Kabwe katika uzinduzi wa “Operesheni Linda Demokrasia Nchini”.
Ndugu
Wananchi, Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwenu kuitikia wito wetu wa
kuja kutusikiliza. Tumewaita hapa ili kuwaeleza kinachoendelea katika
nchi yetu hivi sasa na madhara makubwa yanayoweza kutokea iwapo
hatutosimama kidete dhidi ya mbinu zozote za kufifiza na kuminya
demokrasia na misingi ya uwajibikaji katika nchi yetu.
Mwaka
2015 tulikwenda kwenye uchaguzi kuchagua madiwani, wabunge na Rais.
Baada ya Uchaguzi kumalizika Serikali mpya iliundwa na Serikali za Mitaa
(Halmashauri) kuundwa. Nawapongeza wananchi wote kwa kuendesha zoezi la
uchaguzi kwa amani na kuweka heshima ya nchi yetu mbele.
Baada
ya uchaguzi tumeona viongozi wapya wakichukua hatua mbalimbali nzuri na
mbaya, zenye kujenga na kubomoa, zenye kuimarisha demokrasia na
zinazobomoa demokrasia. Tumeshuhudia maamuzi mengine ambayo yanatia
khofu, kwamba ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na Ufisadi,
lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza Demokrasia ya nchi
yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu.
Mkutano
wetu wa leo utagusia baadhi ya maeneo ambayo tunadhani ni vihatarishi
vya ustawi wa wananchi wetu na ambavyo lazima tuanze kuvipinga mapema
sana kabla havijaota mizizi. Ndugu Wananchi, Baadhi ya maeneo
tutakayozungumza leo ni pamoja na;
- Wabunge kusimamishwa kazi za Bunge
- Maamuzi ya Serikali kuhusu Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
- Hali ya Zanzibar
- Mwelekeo wa Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli
- Tishio la Nchi kuelekea kwenye Utawala wa Imla wa MTU mmoja
Wabunge Kusimamishwa Kazi.
Ndugu
Wananchi, mnamo tarehe 30 Mei, 2016 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, chini ya Naibu Spika lilipitisha Azimio la Bunge la
kuwasimamisha kazi wabunge 7 kwa vipindi mbalimbali. Wabunge wawili,
ndugu Esther Bulaya na ndugu Tundu Lissu walisimamishwa Mikutano miwili
ya Bunge. Wabunge Wanne, ndugu Halima Mdee, Ndugu Pauline Gekul, Ndugu
Godbless Lema na Mimi ninayezungumza nanyi tulisimamishwa mkutano mmoja,
huu unaoendelea wa Bajeti, na mbunge mmoja ndg John Heche Suguta
amesimamishwa vikao 10 vya mkutano huu wa tatu unaoendelea.
Sababu
iliyoelezwa na Bunge ni kwamba wabunge hawa walifanya fujo siku ya
tarehe 27 Januari, 2016 kufuatia hoja niliyoitoa Bungeni ya kutaka
mjadala kuhusu sababu za hovyo na za uongo zilizotolewa na Serikali
kuhusu uamuzi wa kuzuia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na
televisheni binafsi (Star tv na Azam) kuonyesha moja kwa moja mikutano
ya Bunge.
Ndugu
Wananchi, mimi binafsi pamoja na wabunge wengine 6 hatukufanya fujo
yeyote ndani ya Bunge. Kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji maamuzi ya
Serikali ambayo kwa maoni yetu hayana msingi wowote. Serikali inasema
ninyi Wananchi hamfanyi kazi kwa sababu Bunge linaonyeshwa wakati wa
kazi. Hata hivyo Serikali hiyo hiyo inatwambia kuwa katika kipindi cha
miaka 10 iliyopita uchumi wa Tanzania ulikua kutoka tshs 16 trilioni
mwaka 2005 mpaka tshs 99 trilioni mwaka 2015. Kipindi chote hiki Bunge
lilikuwa linaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa (TBC) na
televisheni ya StarTV.
Kama
mngekuwa hamfanyi kazi Uchumi usingekua kwa kiwango hicho cha asilimia
600 ndani ya Muongo mmoja wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Utawala wa
Rais John Magufuli unataka kutuaminisha kuwa ukiwa na Bunge ‘live’ watu
hawafanyi kazi lakini uongozi uliopita umedhihirisha kwa ushahidi kuwa
ukipanua demokrasia na kuwaonyesha wananchi kila kinachoendelea Bungeni
uwezo wa kazi unaongezeka na uwezo wa wananchi kuwajibisha viongozi wao
unaongezeka.
Hivyo
Serikali kuamua kuficha Bunge ni mbinu za kuendesha Serikali kwenye
giza ili kufanya maamuzi ambayo baadaye ionekane Serikali tu au Rais tu
ndiye mfanya kazi. Ndio maana mikutano yote ya Rais anapohutubia
huonyeshwa moja kwa moja lakini sio Bunge.
Wananchi,
Wabunge wamesimamishwa kwa sababu ya kukataa Bunge kuendeshwa kwenye
giza. Wabunge waliosimamishwa walisimama kidete kuhoji sababu za
Serikali kufikia maamuzi hayo. Walitaka kujua kwanini Serikali imekuwa
kigeugeu kwa kubadilisha badilisha sababu zake za kuzuia matangazo ya
moja kwa moja ya Bunge.
Wakati
mmoja Serikali ilisema sababu ni gharama, kama ni hivyo ni kwanini
walizuia StarTV na AzamTV kuonyesha moja kwa moja? Ni dhahiri wananchi
Serikali inataka kuendesha mambo yake kwa uficho kwa sababu kuna maamuzi
inataka kufanya na haitaki wananchi mjue mapema maamuzi hayo. Serikali
inaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele.
Wananchi,
wabunge waliosimamishwa ni wabunge wenye uwezo wa kujenga hoja. Kuna
wengine wamebaki Bungeni wenye uwezo mkubwa tu wa kujenga hoja, lakini
hawa saba waliosimamishwa ni wabunge waliojidhihirisha kwa muda mfupi
kwa baadhi yao kama ndugu Heche, kwamba wanaweza kusimamia hoja zao bila
woga. Swali la kujiuliza ni, tukio ambalo limetokea mwezi Januari ni
kwanini lifanyiwe mwezi Juni tena wiki moja tu kabla ya Waziri wa Fedha
kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali?
Katika
waliosimamishwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Fedha, ndg. Halima Mdee
na Waziri Kivuli wa zamani wa Fedha ambaye anazungumza nanyi leo (Zitto
Kabwe). Kuna nini? Nitawaeleza katika hoja ya Bajeti. Kimsingi Utawala
wa Rais Magufuli umepanga kupandisha kodi za wananchi masikini na uliona
uwepo wetu bungeni utatibua mipango yao.
Rais
na wenzake ndani ya CCM hawapendi kusikia hoja zinazowapinga, hawana
uvumilivu wa kukosolewa na hivyo walipanga kuhakikisha kuwa baadhi yetu
hatutakuwepo kwenye mjadala wa Bajeti ili kufanikisha malengo yao ya
kufanya maamuzi yatakayowandamiza wananchi.
Nitaeleza
vizuri hili baada ya muda kidogo. Hivyo nataka Watanzania wajue kuwa
kusimamishwa kwetu ni ajenda maalumu ya Serikali ya Rais Magufuli
kufunika mjadala wa Bajeti kwa sababu inajua kuwa tunajua inachopanga
kufanya dhidi ya mafukara wa nchi yetu.
Sisi hatutakaa kimya, tutatumia wenzetu waliopo Bungeni kuyasema haya na pia tutazungumza na wananchi kuwaeleza pia.
Tutatumia
mikutano yetu mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyetu kuhakikisha
kuwa Wananchi wanajua kila kinachoendelea na kuwataka kuunganisha nguvu
kukataa udikteta unaonyemelea nchi yetu.
Wanafunzi 7800 Kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma.
Ndugu
Wananchi, mmesikia sakata la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
waliokuwa wanasomea programu maalumu ya Ualimu wa Sayansi. Hawa ni
watoto wa Watanzania masikini waliokubali kuacha kwenda Kidato cha Tano
na cha Sita (A level) na kukubali kusomea diploma ya Ualimu ili
wakawafundishe watoto wa masikini wenzao. Wanafunzi hawa hawakuanzisha
wao program hii, ilianzishwa na Serikali na kupitishwa na Baraza la
Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe na alishiriki kikao hicho
kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri.
Rais
Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama Wenzake walivyofanya
na kuanza kutekelezwa. Lengo na program hii ni kuondoa tatizo la walimu
wa masomo ya Sayansi. Tanzania ina uhaba wa walimu wa Sayansi 26,000
(Kwa Utafiti wa Mwaka 2014) na tukienda kwa utaratibu wa kawaida
tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.
Program
hii ilianzishwa ili kuziba pengo hili kwa muda mfupi, na vijana
waliitikia wito huu wa kizalendo kuhakikisha wadogo zao hawakosi walimu
siku za usoni. Serikali ya awamu ya Tano imewafukuza vijana hawa 7800
kutoka chuoni ndani ya masaa 24 kwa makosa ambayo sio yao.
Wananchi,
hatusemi kuwa program haikuwa na kosoro. Zilikuwepo ikiwemo kudahili
wanafunzi wengi zaidi ya ilivyotarajiwa na kudahili wanafunzi 88 kati ya
7800 ambao walikuwa na daraja la nne (Div 4) katika masomo yao. Lakini
aliyedahili sio watoto hawa bali ni Serikali yenyewe, kwanini waadhibiwe
watoto?
Bunge
lilipotaka kujadili hoja hii au hata kuipeleka kwenye kamati ya Bunge
kuifanyia uchunguzi na kutoa mapendekezo Naibu Spika alizuia hoja ya
mbunge Joshua Nasari bila sababu za msingi. Wabunge wote bila kujali
vyama vyao walitaka hoja ijadiliwe na kuweza kupata majawabu. Mbona
wakati wa Uongozi wa awamu ya 4 tulijadili hoja ya mgomo wa madaktari na
kisha kupelekwa kwenye kamati ya husika ya bunge kupata suluhisho la
kudumu? Kwanini Utawala wa Rais Magufuli hautaki Bunge lifanye kazi
yake? Mbona yeye Rais kaenda kujadili jambo hilo huko Chuo Kikuu
mlimani?
Wananchi,
Rais Magufuli anafikia kuita watoto wetu Vilaza? Rais huyu anayesema
yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini Vilaza. Vijana hawa
Wazalendo waliojitoa muhanga kuacha kwenda kidato cha Tano ili wasome
kuwa Walimu na kulea kizazi kijacho Rais wao anawaita vilaza. Rais sifa
zimempanda kichwani. Rais Magufuli hana budi kuwaomba radhi vijana hawa
na wazazi wao.
Kitaaluma
Rais ni Mwalimu, anajua madhara ya kisaikolojia kufuatia maneno
aliyoyasema. Ni sawa na Jenerali wa Jeshi anayetukana askari wake walio
Mstari wa mbele. Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi
Vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani.
Rais
Magufuli anaongea mno, sio sawa kwa Kiongozi. Rais ajue kuweka akiba ya
maneno. Yeye ni Kiongozi wa wote, wenye akili na Vilaza. Yeye anapaswa
kuwa wa mwisho kuongea ili watu waweze Kukata rufaa kwake. Yeye
akishaongea wananchi ‘aggrieved’ (walioonewa Au kukosewa) waende kwa
nani? Waende kwa mungu?
Tunamtaka
Rais awarudishe wanafunzi Hawa Chuoni mara moja na wale wanafunzi ambao
itaonekana hawakuingia kwenye programu kihalali (ambao Ni 88 Tu)
waondolewe badala ya kuadhibu watoto wote kwa makosa ya wachache ambao
ni asilimia 5 tu ya wote.
Makosa
madogo ni mambo ya kawaida katika Jamii. Yeye Rais ni mfano mzuri wa
hili kwani naye mbona aliteua Waziri mlevi na kurekebisha kwa kumfukuza
peke yake?, mbona hakufukuza Baraza zima la mawaziri kwa ulevi wa Waziri
mmoja?
Zanzibar.
Ndugu
Wananchi mnajua mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kufutwa chama
chetu kiliweka msimamo wa wazi kwamba kinatambua ushindi wa Maalim Seif
Sharif Hamad kama Rais aliyechaguliwa na Wazanzibari na anayepaswa kula
kiapo na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Tuliandika
pia masuala 10 muhimu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuyafanyia kazi, na moja ya jambo tulilomtaka Rais Magufuli Kulifanyia
kazi ni suala la demokrasia ya Zanzibar.
Rais
hakusikia wito wetu na aliruhusu ufutwaji usio halali, kisiasa wala
kisheria wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015.
Tunarudia
kusisitiza kuwa Chama chetu cha ACT Wazalendo hakiutambui uchaguzi wa
marudio wa Zanzibar uliofanyika mwezi Machi mwaka 2016 pamoja na matokeo
yake yote. Kwa maana hiyo hatutambui Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,
Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na Pia Rais wa
Zanzibar.
Wananchi,
Hivi karibuni kumekuwa na kuongezeka kwa sintofahamu huko Zanzibar
kufuatia Mgombea Urais aliyeshinda na kunyanganywa ushindi wake kwenda
kwa wananchi kuzungumza nao.
Hali
hii imepelekea jeshi la polisi kumhoji Maalim Seif na siku mbili
baadaye Dkt. Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu “Hana
vifaru na mizinga”.
Tunalaani
kauli hii ya Dkt. Shein ya kutisha kwa vifaru na mizinga. Kamwe huwezi
kuzima haki za Wananchi kwa vifaru na mizinga. Dkt Shein akumbuke kuwa
Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa Dola kubwa kama
Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.
Dkt
Shein akumbuke kuwa nchi kadhaa duniani zilikuwa na madikteta wenye
vifaru na mizinga lakini waliondoka. Dkt Shein afute kauli yake hii na
kuacha vitisho badala yake aanze mchakato wa kupata maridhiano ya jamii
ya Zanzibar. Hatutaki kurithi damu, tunataka kurithi nchi yenye amani,
haki na demokrasia.
Wananchi,
sisi ACT Wazalendo, tunajua hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar na
mkwamo uliopo hivi sasa Kisiasa, Kijamii na Kiuchumi. Hata hivyo ni
lazima tupate jawabu kupitia sanduku la kura.
Tunapendekeza
kuwa Vyama vikuu vya siasa Zanzibar vikubali ‘kufa kidogo’ yaani ‘to
die a little’, kwa vyote kukubali kuwa Chaguzi zote Mbili, wa Mwaka 2015
na ule wa mwaka 2016 zilikuwa batili, zifutwe na Uchaguzi Mkuu mpya
uitishwe.
Uchaguzi
huo utanguliwe na Serikali ya Mpito itakayohusisha vyama vyote vya
siasa na baadhi ya wanajamii wanaoheshimika na Wazanzibari wote ili
kujenga kuaminiana.
Tunadhani
hii itatupa nusra kwa Zanzibar. Tunawaomba Wazanzibari watumie mwezi
mtukufu wa Ramadhani kutafakari maoni haya na wote kwa pamoja baada ya
Ramadhani kuja na jawabu ya hali ya kisiasa. Tunatamani Zanzibari irudi
kwenye hali ya kawaida na ishamiri.
Zanzibar
ikiingia kwenye mtafuruku Tanzania nzima itakuwa kwenye mtafaruku. Ni
dhahiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kutoa uongozi kwenye suala hili na
hivyo ni wajibu wa Wazanzibari wenyewe kukaa na kupata mwafaka wa
kijamii na kusonga mbele.
Bajeti ya 2016/17.
Wananchi,
kuanzia tarehe 8 mwezi Juni, 2016 Bunge litakuwa kwenye mjadala wa
Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli. Rais ameleta mapendekezo
ya Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni. Katika makadirio haya vyanzo vya
ndani ni shilingi 18.5 trilioni na misaada ni shilingi 3.6 trilioni.
Serikali inatarajiwa kukopa jumla ya shilingi 7.4 trilioni.
Mwaka
2015/16 Serikali ilitarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 13.8 trilioni,
hivyo ndani ya mwaka mmoja wa fedha Utawala wa Rais Magufuli unataka
kukusanya shilingi 4.7 trilioni zaidi sawa na ongezeko la asilimia 25.
Kwa ufupi ni kwamba Serikali haina budi kuongeza kodi kwa kiwango cha
asilimia 25 ili kuweza kutimiza malengo yake ya makusanyo.
Wananchi,
mtakumbuka kuwa mara baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani tulikuwa
tunaelezwa kodi iliyokusanywa kila mwezi na tuliona wafanyabiashara
wakikabwa koo kwa kukwepa kodi. Hata hivyo ongezeko la Makusanyo
lilikuwa kwa miezi 2 tu ya Novemba na Disemba kwani kuanzia mwezi
Janauri makusanyo yalianza kuendana na hali halisi ya uchumi wa nchi
yetu na ndio maana mbwembwe za makusanyo hazisikiki tena hapa nchini.
Ukweli
ni kwamba Rais alikuwa anakusanya ‘arrears’ na hapakuwa na hapajakuwa
na mbinu mpya za kukusanya mapato ya Serikali. Maeneo muhimu
yanayopoteza mapato kama vile makampuni ya nje kutumia mbinu za kihasibu
kukwepa kodi hayajatazamwa kabisa na Rais na wasaidizi wake.
Hivyo,
Serikali imeamua kurudi kwa wanyonge kuwaminya na kodi ikianzia
kuchukua kodi zote za Majengo kutoka kwenye Halmashauri zetu. Kodi za
majengo ndio chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri zetu za Miji,
Manispaa na Majiji. Uamuzi wa Serikali kuchukua chanzo hiki cha mapato
utapelekea Halmashauri zetu kushindwa kuzoa taka na hata kutoa huduma
kwa wananchi.
Hata
hivyo wananchi uamuzi huu ni kwa sababu Halmashauri nyingi za Miji
zinaongozwa na vyama vya Upinzani kama vile Manispaa ya Kigoma Ujiji,
Manispaa ya Iringa, Arusha jiji, Ilala, Kinondoni, Mbeya Jiji nk.
Utawala wa Rais Magufuli unataka kuhakikisha kuwa Manispaa zinaoongozwa
na vyama vya upinzani zinashindwa kutoa huduma. Duniani kote kodi za
majengo hukusanywa na Serikali za Mitaa. Katika Bajeti ya mwaka huu kodi
hizi zitaongezwa maradufu.
Wananchi,
Serikali inatarajia kupandisha ushuru kwenye soda, vilevi na sigara pia
kwa mujibu wa vitabu vya Bajeti vilivyogawiwa kwa wabunge. Hata kodi
kwenye gharama za kupiga simu zitaongezwa kwa zaidi ya asilimia 10. Eneo
la ushuru peke yake Serikali inataka kukusanya shilingi 1.2 trilioni
kutoka shilingi bilioni 900 za mwaka uliopita. Hii ni nyongeza ya
shilingi 300 bilioni zaidi kutoka Bajeti ya mwaka 2015/16.
Maeneo
haya mawili peke yake (kodi za majengo na ushuru wa bidhaa)
yataongezewa kodi kiwango cha kuumiza sana wananchi wa kawaida. Hii ndio
sababu Serikali imefukuza baadhi ya wabunge mahiri bungeni ili
kulainisha upitishwaji wao wa viwango hivi vya kodi. Hata hivyo
tutatumia wabunge waliobakia Bungeni kuhakikisha kuwa kodi kwa wananchi
masikini haziongezwi kiholela.
Wananchi,
sisi tunaamini kuwa Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni ya Utawala wa
Magufuli sio bajeti halisi kwani makadirio yao hayazingatii ukuaji wa
uchumi na yana lengo la kuchukua fedha kutoka kwa wananchi kupeleka
Serikali jambo ambalo litadidimiza uchumi wa nchi yetu.
Tishio la Demokrasia.
Wananchi
jambo la mwisho ambalo ninataka kuwaeleza ni tishio lililopo mbele yetu
dhidi ya demokrasia ya vyama vingi. Hatua mbalimbali ambazo Utawala wa
Rais Magufuli unachukua ni ishara ya kutengeneza utawala wa Kiimla. Rais
ndiye anayejua kila kitu na ndiye anayeamua kila kitu. Hii ni hatari
sana kwa nchi yetu na ni lazima kuchukua hatua mahususi kumkatalia Rais
mwanzoni kabisa ili asizoee.
Tunarudia
kuwa tulimuunga mkono Rais toka mwanzo katika vita dhidi ya Ufisadi,
kwani ni vita muhimu na lazima ipiganwe bila kujali itikadi za vyama.
Hakuna namna unaweza kumlaumu Rais anapochukua hatua za kusafisha Uvundo
katika nchi. Tutaendelea kumwunga mkono katika eneo hilo.
Wananchi,
hata hivyo Rais anatia Khofu mno katika ujenzi wa mfumo wa uwajibikaji.
Tanzania ina vyombo vya kuimarisha uwajibikaji, ikiwemo Bunge la
Jamhuri ya Muungano na Pia Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa. Rais anataka
kupigana dhidi ya ufisadi nje ya mfumo jambo ambalo ni la hatari sana
kwa nchi kwani akitoka yeye tutaanza upya.
Inawezekanaje
Kiongozi anayepambana na rushwa akavunja nguvu ofisi ya ukaguzi ya
Taifa kwa kumnyima Bajeti Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG)? Rais amediriki
hata kuvunja Katiba na sheria ya ukaguzi, kwani Bajeti ya CAG haipangwi
na Serikali bali hupangwa na Kamati ya Bunge. Rais ameenda kinyume na
sheria na badala yake kapanga mwenyewe Bajeti ya CAG? Toka lini
mkaguliwa akapanga bajeti ya anayemkagua? Kamati ya Bunge ilipanga
Bajeti ya tshs 69 bilioni kwa CAG lakini Serikali (mkaguliwa) imeipiga
panga mpaka tshs 32 bilioni. Hii ni moja ya mfano dhahiri kabisa wa
Serikali kuanza kuvunjavunja vyombo vya uwajibikaji.
Wananchi,
hivi sasa kuna Ukosefu wa Sukari nchini. Rais alisimama kwenye Vilinge
vya Siasa, akatoa matamko makali kwamba kuna Wafanyabiasha wameficha
sukari na tukaonyeshwa sukari hiyo. Hata hivyo baada ya siku chache
vyombo kama PCCB na TRA vikasema sukari ile ni halali. Inakuwaje Rais
alitamka maneno yale bila ya kushauriana na vyombo? Ni dhahiri Rais
anaongea na kuropoka tu na kutaka kujenga utawala wa Kimla. Leo bado
kuna shida ya sukari na sukari ambayo serikali inasema iliagiza
haionekani. Ipo wapi?
Wananchi,
Rais Huyu Huyu alikwenda Benki Kuu na kusema nusu ya wafanyakazi pale
ni hewa. Mpaka leo hatujaona hao wafanyakazi hewa wa BoT. Rais alikwenda
tu kwa kupata maneno ya kuokoteza barabarani na kutoa matamko ambayo
yanashusha hadhi ya Benki, lakini Rais anashindwa kutoka mbele kusema
alikosea. Tunajenga mfumo mbaya sana wa uongozi wa Nchi.
Leo
tunataka kumwambia Rais kuwa aongoze, asitawale. Rais awe na Utu na
wananchi wake. Rais awe anasikiliza kwanza na kuchambua mambo kabla ya
kusema chochote mbele ya hadhara. Rais awe wa mwisho kusema ili kama
kuna rufaa Watu waseme kwake. Vinginevyo Rais anataka kujenga utawala wa
Kiimla, tutamkatalia wazi wazi.
Wananchi,
nimalizie kwa kusema yafuatayo. Rais John Magufuli amesema kuwa yeye
amejitoa muhanga kupambana na ufisadi. Sisi tunalazimika kujitoa muhanga
Kulinda Demokrasia.
Ni
imani yetu kuwa Ufisadi utapigwa vita kikamilifu sio kwa kutegemea nia
ya mtu mmoja bali kwa kuboresha na kutumia misingi ya demokrasia kwa
kujenga taasisi madhubuti zitakazomaliza janga la ufisadi bila ya
kutegemea nia ya Rais.
Sisi
tunaamini kuwa ni jukumu letu kusimama kujitoa mhanga kuzuia maafa ya
kitaifa yatakayoweza kutokea kutokana na makosa ya kukandamiza
demokrasia na uhuru wa mawazo kwa kuhoji, kukosoa na kurekebisha makosa
hayo sasa bila kuchelewa.
Tunamwunga
mkono Rais kutokomeza Ufisadi lakini TUNAMPINGA Rais Kutokomeza
Demokrasia. Demokrasia yenye misingi madhubuti ya Uwajibikaji ndio
jawabu sahihi dhidi ya ufisadi na unyonyaji nchini kwetu.
Nawashukuru sana.
Zitto Ruyagwa Kabwe
Dar es Salaam
Juni 5, 2016
No comments