Ugonjwa wa ajabu wazuka Dodoma, waua watu 7, wengine 21 wamelazwa
Ugonjwa huo uliozuka katika wilaya za Chemba na Kondoa hadi sasa umesababisha vifo vya watu 7 huku 21 wakiwa wamelazwa hospitalini na wawili kati yao ni watoto ambao hali yao si nzuri sana.
Kufutia madai ya watu kusema kuwa ugonjwa huo huenda ukawa ni Kimeta, serikali imekanusha taarifa hizo kuwa si kweli kuwa ugonjwa huo ni Kimeta kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ugonjwa huo ulianzia katika wilaya ya Chemba ambako watu tisa wa familia moja kutoka kijiji cha Mwaikisabe kata ya Kihama, waliathirika na baadaye wagonjwa wengine walianza kupatikana kutoka vijiji vya karibu.
Kilicho chakushtua zaidi ni baada ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Dodoma kueleza kuwa ugonjwa huo umeua baadhi ya mifugo huku akieleza dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kuharisha, kupata maumivu makali ya tumbo, kutapika matapishi ya rangi ya nyeusi, kupata choo cheusi na macho kuwa ya njano.
Taarifa za awali za chanzo cha ugonjwa huo zinaelezwa kuwa ni watu kula nyama ya ng’ombe aliyechinjwa baada ya kuvunjika mguu, ingawa baaadhi ya watu waliokula nyama ya ng’ombe huyo hawajaugua hivyo kuzua maswai kama kweli nyama ya ng’ombe huyo ndiyo tatizo.
No comments