Rufani ya Jamhuri Dhidi ya Bosi wa Zamani wa TRA na Wezake Kusikilzwa Jumanne ya Wiki Ijayo
Mahakama ya Rufani imepanga kusikiliza rufaa dhidi ya Mwenyekiti wa
kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry
Kitilya na wenzake, Shose Sinare na Sioi Solomon juma lijalo.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka Mahakama ya Rufani, rufaa hiyo imepangwa
kusikilizwa Jumanne Mei 31 na chini ya majaji watatu Bernard Luanda, Salum
Masatti na Semistocles Kaijage.
Rufaa hiyo ilifunguliwa na
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupa
rufaa yake ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuwafutia washtakiwa hao
shtaka la kutakatisha fedha.
Kitilya na wenzake walikuwa
wakikabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za
uongo kwa mamlaka za Serikali, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu
na kutakatisha Dola za Marekani 6 milioni.
Hata hivyo, baadaye
Mahakama ya Kisutu iliwafutia shtaka la kutakatisha fedha, baada ya
mawakili wa washtakiwa hao kupinga uhalali wa shtaka hilo, uamuzi huo
ulipingwa na DPP na kukata rufaa Mahakama Kuu akipinga uamuzi wa
Mahakama ya Kisutu, lakini mawakili wa washtakiwa hao waliweka pingamizi
wakidai kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu hauwezi kukatiwa rufaa kwa
kuwa ni uamuzi mdogo ambao haumalizi kesi.
Mahakama Kuu katika
uamuzi wake uliotolewa na Jaji Moses Mzuna, ilikubaliana na pingamizi la
mawakili wa washtakiwa hao na ikaitupa rufaa hiyo na kuelekeza DPP
arudi Mahakama Kisutu aombe kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka
ili kurekebisha shtaka la kutatakisha fedha lililofutwa.
DPP hakuridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama Kuu ndipo akaamua kusonga mbele na kukata rufaa nyingine Mahakama ya Rufani.
Kitilya
na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya
Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za
Marekani 550 milioni kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya
Uingereza.
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Rufani imefufua
kesi ya uchaguzi dhidi ya Mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya, Haroun Mullah
iliyokuwa imetupwa na Mahakama Kuu na kuamuru isikilizwe upya.
Mahakama
ya Rufani imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya katika uamuzi wake wa
rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa mpinzani wake wa karibu katika
kinyang’anyiro Uchaguzi Mkuu 2015, Liberatus Laurent Mwang’ombe.
Mwang’ombe alikata rufaa hiyo baada ya kesi yake ya msingi ya kupinga
matokeo yaliyompa ushindi Mullah kutupwa na Mahakama Kuu, kutokana na
kutokuwasilisha baadhi ya vielelezo vya ushahidi wa kesi yake.
Mahakama
Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Atuganile Ngwale, ilisema
kutokana na kutokuwapo vielelezo hivyo ambavyo ni fomu ya matokeo na
kadi ya gari la mdaiwa (Mbunge Mullah) kunaifanya kesi hiyo kukosa
msingi wa sababu za madai.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani
ilisema kuwa Mahakama Kuu ilikosea kuitupa kesi hiyo, kwani ilikuwa bado
katika hatua za awali na ilikuwa haijaanza kusikilizwa, hivyo mdai
alikuwa na nafasi ya kuwasilisha vielelezo hivyo.
Hivyo,
Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa juzi na majaji watatu
Engela Kileo, Katherine Oriyo na Semistocles Kaijage, iliamua kesi hiyo
isikilizwe upya.
No comments