Baada ya kuifunga Atletico Madrid fainali, Real Madrid wamefikisha jumla ya Makombe 11 ya UEFA
Usiku wa May 28 2016 wapenda soka wote duniani macho na masikio yao ilikuwa ni katika uwanja wa San Siro katika jiji la Milan Italia, ili kutaka kufahamu nani atafanikiwa kuchukua Kombe la Klabu Bingwa Ulaya 2016 kati ya Real Madrid na Atletico Madrid.
Real Madrid ambao wanatajwa kama klabu yenye mafanikio katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, wameifunga Atletico Madrid kwa jumla ya penati 5-3, hiyo inatokana na dakika 120 za mchezo kumalizika kwa sare ya goli 1-1, magoli ambayo yalifungwa na Sergio Ramos dakika ya 15 kwa upande wa Real, wakati goli la Atletico lilifungwa na Ferreira Carrasco dakika ya 79.
Kwa upande wa Atletico wanakuwa na bahati mbaya kutokana na kutofanikiwa kuweka rekodi ya kutwaa Kombe hilo kwa mara ya kwanza, lakini kwa upande wa Real Madrid hilo linakuwa Kombe lao la 11 la Klabu Bingwa Ulaya, takwimu na bahati zimeendelea kuwa rafiki zaidi kwa Real Madrid kuliko Atletico.
Mchezo huo toka awali ilionekana kama Atletico Madrid hawana bahati, kutokana na kupoteza nafasi ya adhabu ya mkwaju wa penati waliyokuwa wamepewa, lakini Antoine Griezmann akakosa penati hiyo dakika ya 48 ya mchezo, Juanfran ndio mchezaji pekee wa Atletico Madrid aliyekosa penati.
No comments