Makandarasi 4572 Wafutiwa Leseni Nchini
Bodi
ya Usajili wa Makandarasi imefuta usajili wa jumla ya makandarasi 4572
kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Sheria ya Usajili wa Makandarasi ya
mwaka 1997.
Hayo
yamebainishwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB),
Bw. Rhoben Nkhori wakati wa Mkutano wa Mashauriano wa CRB uliofanyika
jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bw.
Nkhori amesema kuwa katika jukumu la kuratibu mwenendo wa kazi za
makandarasi, Bodi ilikagua miradi 2735. Katika miradi hiyo
iliyokaguliwa, miradi 1873 sawa na asilimia 68.5 haikuwa na kasoro.
Ameongeza
kuwa miradi mingine ilikuwa na kasoro za kutofanywa na makandarasi
waliosajiliwa, kutozingatia usalama wa wafanyakazi, kutokuwa na bango
wala uzio na miradi kutosajiliwa. Kwa mujibu wa Bw. Nkhori miradi yote
iliyopatikana na upungufu wahusika walichukuliwa hatua mbali mbali kwa
mujibu wa sheria.
Aidha,
Bwana Nkhori amesema kuwa kwa mwaka jana, Bodi ilisajili miradi 3,172
yenye thamani ya shilingi trilioni4.23. Katika miradi hii asilimia 44.4
ilifanywa na Makandarasi wazawa na asilimia 55.6 ilifanywa na
makandarasi wa kigeni.
Licha
ya mafanikio hayo CRD ilikumbana changamoto kadhaa ikiwemo kuwasilisha
nyaraka za kugushi wakati wa usajili hususani kadi za magari na mitambo,
vyeti vya wataalam, kutumia majina ya makandarasi kwa udanganyifu kwa
kuuza vibao, waendelezaji kutotoa taarifa sahihi za umiliki kwa Bodi na
baadhi ya makandarasi kushindwa kuwalipa wafanyakazi na vifaa vya
ujenzi.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Bi Consolata
Ngimbwa amemwomba Mhe. Rais John Pombe Magufuli kuwapa kipaumbele
Makandarasi wa humu nchini ili kuwawezesha kiuchumi. “Mhe. Rais tunaomba
utupe kipaumbele kwani sisi tukipata hiyo miradi tutawekeza hapa nchi
na kuongeza soko la ajira,”alisema Bi Ngimbwa.
Katika
hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania amesema serikali yake itawapa kipaumbele
makandarasi wazawa lakini akawataka wajipange na kufanya kazi kwa weledi
na kuzingatia maadili ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Mkutano
huu pamoja na mamabo mengine utajadili jinsi ya kuwajengea uwezo
makandarasi nchini. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Juhudi za Makusudi za
kukuza uwezo wa makandarasi wazawa, changamoto na mustakhabali.”
No comments