Profesa Anna Tibaijuka kitanzini Tena......Katuhumiwia Kujimilikisha Shamba la Hekari 4,000
Mbunge
wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk
Charles Mlingwa wamelipuliwa bungeni wakidaiwa kutumia madaraka yao
vibaya.
Tuhuma
hizo zilitolewa jana na wabunge wa upinzani Conchesta Rwamlaza (Viti
Maalum - Chadema) na Dk Godwin Mollel (Siha - Chadema) walipokuwa
wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Rwamlaza
alidai kuwa katika Kijiji cha Kamwila wilayani Muleba, Profesa
Tibaijuka akiwa serikalini, aliomba eka 1,098 lakini hivi sasa anamiliki
eka 4,000 jambo ambalo linazua mgogoro na wananchi.
“Hili linaleta matatizo kwa kuwa haiwezekani mtu awe na eneo hilo lote halafu anakodisha kwa wananchi,” alisema Rwamlaza.
Alisema
kuna haja ya kwenda kupima ardhi hiyo na kama Profesa Tibaijuka aliomba
heka 1,098 apewe hizo na si kumiliki eka 4,000 alizonazo hivi sasa.
Dk Mollel alimtaka Waziri Mkuu amhamishe Dk Mlingwa akidai ni tatizo katika wilaya hiyo.
Alisema juzi ulitokea mgogoro kati ya wananchi wa Arumeru na Siha katika mpaka jambo lilisababisha kubomoleana nyumba.
“Mkuu wa Wilaya alifika pale akiwa amelewa na kusababisha wananchi kuchukua hatua hizo wakati ilitakiwa tu tutumie akili,” alisema Dk Mollel.
Dk
Mollel alisema kama DC huyo ataendelea kuwa na tabia hiyo, migogoro
haitaisha na wawekezaji hawatawaheshimu wananchi kwa kuwa kiongozi wao
anawaaibisha.
“Kama
hamtamtoa huyu DC ambaye anatuaibisha kwa kuomba vitu vidogovidogo kwa
wawekezaji basi sisi tutamtoa kwa kuwa hatuhitaji aibu.”
Alisema
kuna haja ya kwenda kupima ardhi hiyo na kama Profesa Tibaijuka aliomba
eka 1,098 apewe hizo na si kumiliki eka 4,000 alizo nazo hivi sasa.
Dk Mlingwa ajibu tuhuma
Akizungumzia
tuhuma hizo, Dk Mlingwa alisema tangu kipindi cha kampeni, mbunge huyo
alikuwa akimshambulia kwa maneno ya uongo ili kupata kura za huruma.
“Hata
hii leo (jana) asubuhi alinitumia meseji akisema ooh nakwenda
kukushtaki kwa Rais na Waziri Mkuu, akaweka na maneno ya vitisho mimi
nikamwambia nenda kwa vile yote ni uongo,” alisema.
“Nadhani
kwa sababu ya ahadi za uongo alizokuwa nazo kuwa akichaguliwa yeye
mashamba yote ya wawekezaji yaliyoko Siha, yatakuwa mikononi mwa
wananchi jambo ambalo haliwezekani.”
Dk
Mlingwa alisema wawekezaji hao wana hati za kumiliki mashamba hayo na
hilo ndilo ambalo Serikali imekuwa ikiwaeleza wananchi ukweli ili
kuepuka propaganda za uongo za mbunge.
“Hiyo
ndiyo imemfanya aendelee kumsema vibaya mkuu wa wilaya na mkurugenzi
katika kila nafasi anayoipata hata hayo aliyoyasema bungeni ameniambia
kwa meseji leo atayasema,” alisema.
“Mkuu wa wilaya kwa bahati nzuri hawezi kujificha tabia na matendo yake kama ningekuwa mlevi wananchi wangeshasema.”
Wabunge
wamemshushia ‘zigo’ la migogoro ya ardhi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakimtaka atatue migogoro hiyo kwa
kasi ambayo ameanza nayo.
Akichangia
hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, jana, Mbunge wa Arumeru Mashariki
(Chadema), Joshua Nassari alizungumzia mgogoro wa ardhi katika Wilaya ya
Arumeru na kusema mgogoro huo umekuwapo tangu mwaka 1993.
Nassari
alinukuu tangazo katika gazeti la Serikali na kusema Rais alitangaza
kufuta umiliki wa shamba hilo. Hata hivyo, alisema mwekezaji huyo
aliendelea kumiliki shamba hilo na kuwakataza wananchi kulima.
“Huyu
Mzungu ni nani? Kwa nini anakuwa na nguvu kuliko Serikali? Rais
alitangaza kufuta umiliki wa shamba hilo tangu mwaka 1993, lakini mpaka
leo anaendelea kumiliki eneo hilo wakati halitumii,” alisema.
Alisema wananchi wanapodai ardhi yao wanafunguliwa kesi za kusingiziwa na kufungwa.
Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM), Bupe Mwakanata alimtaka waziri Lukuvi
kushughulikia mgogoro wa shamba la Efatha, uliodumu kwa muda mrefu bila
kutatuliwa.
“Serikali
iwasaidie wananchi wake kwa kuwarudishia ardhi yao ambayo haitumiki
kikamilifu. Wananchi wa eneo hilo wanategemea kilimo, ukiwanyang’anya
ardhi unawasababishia ugumu wa maisha,” alisema.
Mbunge
wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alizungumzia mgogoro katika eneo
linalozunguka Ziwa Chala. Alisema eneo hilo amepewa mwekezaji ambaye
anawazuia wananchi kutumia maji na kusababisha mgogoro kati ya wananchi
na mwekezaji na kati ya wananchi na Serikali.
“Ziwa
Chala ndiyo pekee ambalo asilimia 85 ya maji yake ni safi na salama na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wako pale kufanya utafiti. Tunaomba umalize
mgogoro huo, ili wananchi watumie ziwa hilo na ardhi kwa ajili ya
kilimo,” alisema Selasini.
Mbunge
wa Mpanda Vijijini (CCM), Moshi Kakoso alisema Mkoa wa Katavi una
migogoro mingi ambayo inasababishwa na mipaka kati ya vijiji hivyo na
Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Alisema
vijiji vya Kapanga, Lugonesi, Kabage na Nkungwi vinakabiliwa na mgogoro
ya ardhi ambayo inawafanya wananchi wa maeneo hayo kushindwa kufanya
shughuli za uzalishaji.
“Ninaomba
wakati waziri anashughulikia migogoro ya ardhi atuangalie na sisi mikoa
ya pembezoni. Tuna migogoro mingi ambayo haijapatiwa ufumbuzi na
Serikali haijafanya jitihada zozote,” alisema.
Mbunge
wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM), Omary Mgumba alisema kumekuwa na
mgogoro kati ya Mkoa wa Morogoro na Pwani kwenye vijiji vya mpakani.
Alimtaka Waziri Lukuvi kutembelea eneo hilo ili mgogoro uishe na wananchi wafanye kazi ya uzalishaji.
Mbunge
wa Karatu (Chadema), Willy Quambalo alisema kuna mwekezaji katika
wilaya hiyo ambaye amepewa ekari 3,850 huku wananchi wakipata shida kwa
sababu ameziba njia ambayo inapita katika eneo hilo.
Wakati
huo huo, Lukuvi amepiga marufuku watu wote wenye mashamba makubwa ambao
wanayapima na kuuza viwanja, waache kwa kuwa haliruhusiwi kuanzia sasa.
“Kama ni shamba litabaki kuwa shamba kama mtu alinunua shamba anataka kubadilisha liwe kiwanja imekula kwake,” alisema Lukuvi na kuongeza kama kuna mtu anataka kufanya hivyo akabidhi shamba kwa halmashauri ili ligawiwe au kuuzwa.
No comments