Bajeti Ya Wizara Ya Maliasili Na Utalii Yapitishwa, Usafirishaji Wa Wanyama Hai Nje Ya Tanzania Wapigwa Marufuku Kwa Miaka 3.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Serikali imesimamisha utoaji wa vibali na uuzaji wa wanyama hai kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 mpaka hapo itakapotangazwa tena.
Serikali imesimamisha utoaji wa vibali na uuzaji wa wanyama hai kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 mpaka hapo itakapotangazwa tena.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametoa agizo hilo bungeni
mjini Dodoma wakati akijibu hoja na michango mbalimbali ya wabunge
iliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa
kiasi cha shilingi bilioni 135.7.
Prof.
Maghembe ameiagiza Idara ya Wanyamapori ipange na kuweka utaratibu mpya
utakaotumika kusimamia biashara hiyo pindi itakaporejeshwa tena baada
ya kumalizika kwa muda wa zuio la Serikali la miaka 3 ikizingatia
mazingira ya uhifadhi wa wanyama hao.
USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI NJE YA NCHI.
Amesema
kumekuwa na taarifa za baadhi ya watanzania wasio waaminifu ambao
wamekua wakijihusisha na vitendo vya kusafirisha wanyama hai
waliokatazwa kinyume cha utaratibu jambo ambalo limeisababishia Serikali
ipoteze mapato kutokana na wanyama hao.
Kuhusu
wanyama wanaoruhusiwa kusafirishwa kama nyani, Kenge,ndege, kobe,
wadudu na tumbili amesema kuwa wamekuwa wakisafirishwa kinyume na
utaratibu na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwa ajili ya
kutumiwa na makampuni ya kimataifa kwenye shughuli za utafiti wa
kisayansi wa tiba na chanjo.
Amesema
makampuni hayo yamekuwa yakinufaika binafsi kwa kupata fedha nyingi
pindi yanapofanikiwa kupata chanjo au tiba husika huku maeneo
waliokotoka yakipata fedha kidogo jambo ambalo serikali ya awamu ya tano
imeamua kulifanyia kazi.
UTALII KUSINI MWA TANZANIA NA MAENEO MENGINE.
Amesema
Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa Utalii wa
Kusini ili kuweka mazingira wezeshi na kuondoa vikwazo vilivyokuwa
vikisababisha watalii kushindwa kufika katika maeneo ya hifadhi za Taifa
eneo la ukanda wa kusini mwa Tanzania.
Baadhi
ya maeneo yatakayoshughulikiwa ni gharama ya usafiri wa ndege kwenda
na kurudi katika maeneo hayo kuwa kubwa hadi kufikia Dola za kimarekani
1800 jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa watalii hao.
Amesema
Serikali itaanzisha vituo vya kuwekea mafuta ya ndege mahali vilipo
vivutio vya utalii ili kuziwezesha ndege ndogo kufika kwa urahisi na
kupata huduma ya kuongeza mafuta ili kupunguza gharama kwa wasafiri
wanaotembelea hifadhi za eneo hilo.
Aidha
amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itanunua ndege ndogo
abiria ili kuwezeha watalii kufika kwa urahisi katika maeneo ya
hifadhiza Taifa.
UTAMBUZI WA MAENEO MAPYA YA UTALII.
Serikali
kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya, mikoa na Wabunge itaanzisha mpango
mpya kuviorodhesha vivutio vyote vya utalii vilivyo katika maeneo yao
ili viweze kutangazwa ipasavyo na kuongeza kuwa mara baada ya kukamilika
kwa mpango huo itaandaliwa orodha ya vivutio hivyo ili vianzwe
kutangazwa rasmi.
Katika
kuimarisha shughuli za utalii nchini serikali itaweka mkazo katika
uimarishaji wa utalii wa utamaduni, uimarishaji wa maeneo ya historia na
Malikale ili kuwezesha eneo hilo kuchangia zaidi katika pato la taifa.
ULINZI NA USALAMA WA HIFADHI ZA TAIFA.
Prof.
Maghembe ameeleza kuwa suala la ulinzi na usalama wa hifadhi zote za
Taifa liko kwa mujibu wa sheria na kubainisha kuwa serikali imeanzisha
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) litakalochukua mbuga
zote zilizokuwa na uongozi ambazo ziko nje ya TANAPA.
Jeshi
hilo litapambana kikamilifu na ujangili, kuimarisha maadili na nidhamu
ya askari wa ulinzi wa hifadhi za taifa pamoja na kushughulikia maslahi
yao na kuondoa migogoro kati ya askari na wananchi.
Amesisitiza
kuwa mara baada ya Bunge la Bajeti, Wizara itakutana na wahifadhi wakuu
wote ili kuweka vigezo vya kuzingatia katika majukumu yao na kusisitiza
kuwa wahifadhi wote watakaoshindwa kwenda na kasi ya vigezo
vilivyowekwa hawatajumuishwa kwenye jeshi hilo.
Aidha,
amekemea vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari wa hifadhi
kupiga raia na kuchoma nyumba za wananchi kuwa havikubaliki na ni
kinyume cha majukumu yao.
”
Nimesikiliza kwa makini michango ya wabunge na nimesikia wafanyakazi
katika hifadhi zetu wanapiga raia wanaua mifugo na kuchoma nyumba za
wananchi jambo ambalo halikubaliki, hatukuwatuma kufanya hivyo” Amesisitiza Prof.Maghembe.
MIGOGORO YA MIPAKA MAENEO YA HIFADHI.
Serikali
imesema mpaka sasa kuna migogoro ya ardhi 281, kati ya hiyo 35 ambayo
ni sawa na asilimia 12.5 ni migogoro ya hifadhi na kuita Mikoa yenye
migogoro hiyo kuwa ni pamoja na Mara , Tanga na Kagera inachukua jumla
ya asilimia 50.
Aidha,
amesema kuwa mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa na eneo kubwa la ardhi
na unaongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya hifadhi kwa asilimia 40.
Katika
kuishughulikia migogoro hiyo Serikali imeziagiza wizara za Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maji na Umwagiliaji, TAMISEMI, Nishati na
Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira pamoja na Wizara ya
Maliasili na Utalii kushirikiana pamoja katika kutatua migogoro yote ya
ardhi nchini.
UBORESHAJI WA MAENEO YA HIFADHI NA MAMLAKA ZA UHIFADHI.
Amesema
katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 1
kimetengwa kushughulikia usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo vya
kisasa katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro vitakavyokuwa na uwezo wa
kugeuza maji taka kuwa poda ili kuweka mazingira yote ya mlima huo kuwa
safi.
Aidha,amesema
kuwa Mamlaka za hifadhi za Taifa zimeendelea kuchangia katika maendeleo
ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa,
miundombinu ya barabara, utoaji wa madawati katika halmashauri
mbalimbali nchini.
No comments