Rais Magufuli Awataka Makandarasi Wazawa Kuwa Wazalendo
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka
wakandarasi kote nchini kufanya kazi kwa kutanguliza maslai ya taifa,
badala ya kutaka kupata faida kubwa kupita kiasi kutoka kwenye zabuni za
miradi ya ujenzi wanayopata kutoka serikalini.
Dkt.
Magufuli amesema hayo leo tarehe 26 Mei, 2016 alipokuwa akifungua
mkutano wa mashauriano wa bodi ya usajili wa wakandarasi kwa mwaka 2016
unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar
es salaam.
Rais
Magufuli amesema serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi
wa Tanzania pale inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, lakini
amewataka kujirekebisha kwa kupanga viwango vinavyostahili vya gharama
za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo serikali itaridhika.
“Nawatolea
mfano, idara ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za
wilaya, kwenye bajeti wana shilingi bilioni 24, makadirio ya kitaalamu
yanaonesha kila jengo lisizidi shilingi milioni 200, wakandarasi
wazalendo walipoomba katika nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwwe
kwa shilingi bilioni 1 na milioni 400, sasa nakuuliza Mheshimiwa
Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo huo
utapasua moyo.
“Hata
kama utakuwa na upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa, sasa
mimi niwaombe ndugu zangu wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali
kuwasaidia wakandarasi wazalendo ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya
kuisadia nchi” Amesema Rais Magufuli
Pamoja
na hilo, Rais Magufuli ametaka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa
watendaji wa serikali pale wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake
amewataka kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa
(TAKUKURU) ili watendaji hao wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Mimi
niwaombe wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji
wanaoomba rushwa, atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na
utakapotoa rushwa huna hakika kama ile tenda utaipata, wengine wameishia
kutoa rushwa hapa, rushwa hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi
huipati na rushwa umeitoa” Amesisitiza Dkt. Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli ametoa wito kwa wakandarasi hao kujipanga ipasavyo ili
waweze kupata zabuni katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi
itakayofanywa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka
Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli
ya Kati na Ujenzi wa Viwanda.
“Sina
uhakika kwamba mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha
hiyo kazi mnaipata ya kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi
Tanga.
“Nitasikitika
sana kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka
Tanzania, wenzetu wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania
wameendelea sana, lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya
kutojua changamoto zinazotukabili, tumejipanga kujenga reli ya kati
(Standard Gauge) kwenye bajeti ya mwaka huu tunaanza na kilometa 100,
lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya China, tutajenga
zaidi ya kilometa 1,200 (Standard Gauge, Central Corridor)
itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda. Wakandarasi wa
Tanzania mmejipangaje? ameuliza Rais Magufuli.
Mkutano
huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ambaye amesema
Taasisi hiyo ipo tayari kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya
ujenzi ambayo ni miongoni mwa sekta zenye rushwa kubwa na ametaka
wakandarasi watoe ushirikiano kukomesha tatizo hilo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Mei, 2016
No comments