MAJI YA MTO YAGEUKA 'RANGI YA DAMU' URUSI
Wachunguzi wa masuala ya mazingira nchini Urusi wanajaribu kubaini sababu iliyoyafanya maji ya mto ulio karibu na kiwanda cha nikeli cha kampuni ya Norilsk Nickel kubadilika na kuwa ya rangi nyekundu.
Picha za maji ya mto Daldykan ambayo yamebadilika rangi zimesambazwa sana katika vyombo vya habari Urusi.
Gazeti la serikali la Rossiiskaya Gazeta linasema kuvuja kwa bomba la kusafirisha taka za mchanganyiko wa shaba nyekundu na nikeli huenda likawa kiini cha maji hayo kubadilika rangi.
Norilsk Nickel ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa nikeli na palladium duniani.
Kampuni hiyo ina vinu na tanuri nyingi rasi ya Taimyr eneo la Krasnoyarsk katika jimbo la Siberia. Ujenzi wa vinu hivyo vikubwa ulifanyika enzi za muungano wa Usovieti.
Kampuni hiyo ina kiwanda kwa jina Nadezhda karibu na mto Daldykan lakini maafisa wake wanasema hawajapata dalili zozote za uchafuzi kutoka kwa kiwanda hicho.
Rais wa kampuni hiyo ni bilionea Vladimir Potanin.
No comments